VITA BARIDI bado inaendelea?

VITA BARIDI bado inaendelea?
Vita Baridi ulikuwa ni ugomvi au mzozo wa kisiasa uliofuatia vita kuu vya pili vya dunia. Ulizihusisha kanda ya mashariki (Urusi na washirika wake Kisovieti) dhidi ya kanda ya Magharibi (Marekani na washirika wake wa NATO).
Wanahistoria wanakitaja kipindi cha vita baridi kuwa ni kuanzia mwaka 1947 hadi 1991, mwaka ambao Jamhuri ya Kisovieti ilipovunjika.
Kwa nini iliitwa Vita Baridi?
Pande zote mbili ziliunda majeshi makubwa na kuwa na silaha nyingi, lakini hazikuanzisha vita moja kwa moja, ila zilijaribu kutishana na kupeana matatizo kwa njia nyingi. Kipindi hiki kilikuwa na maandalizi ya vita lakini vita vya kijeshi havikuanza. Sababu muhimu ya kutoingia katika mapigano ya wazi ilikuwa akiba kubwa ya silaha za nyuklia kila upande na wote walijua ya kwamba vita vingeleta uharibifu mkubwa kabisa kwa nchi zote zilizoshiriki, hata kwa dunia yote.
Chanzo ni nini?
Vita baridi vilianza baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Marekani, Uingereza na Ufaransa zilikuwa nchi washindi wa vita hii dhidi ya Ujerumani. Urusi ulikuwa na siasa ya kikomunisti lakini washindi wengine walifuata siasa ya kidemokrasia pamoja na uchumi wa kibepari. Ikumbukwe kuwa, Urusi ilijitoa kwenye vita vya kwanza vya dunia baada ya kufanya mapinduzi ya Kikomunisti mwaka 1917 hivyo kuachana na ushiriki wa vita hivyo vya mabepari.
Matokeo ya Vita Baridi barani Africa
Maendeleo ya Afrika yaliathiriwa pia na vita baridi. Kwa jumla kila upande ulijaribu kuvuta nchi changa za Afrika upande wake. Kama serikali ilipatana na upande mmoja, upande mwingine mara nyingi ulikuwa tayari kusaidia wapinzani wa ndani kwa msaada wa silaha na pesa.
Wapigania uhuru katika makoloni ya Ureno kama Msumbiji au Angola walipata msaada wa silaha na pesa kutoka nchi za mashariki kwa sababu Ureno ilikuwa nchi ya NATO. Wapinzani hao walitazamwa na magharibi kama Wakomunisti na mawakala wa Wasovyeti, hivyo Marekani ilisaidia Afrika Kusini ingawa siasa ya ubaguzi wa rangi ilivunja haki za binadamu.
Madikteta wengi wa Afrika walipata usaidizi wa upande mmoja au mwingine wakitangaza tu kushikamana nao. Serikali ya Mobutu Sese Seko katika Kongo ilisaidiwa na nchi za magharibi kwa sababu Mobutu alijitangaza kama adui wa Ukomunisti. Haile Mengistu Mariam wa Ethiopia alipata silaha na washauri kutoka upande wa mashariki na polisi ya siri ya Ujerumani ya Mashariki ilitoa ushauri kwa wapelelezi wa Ethiopia jinsi ya kutafuta wapinzani wa ndani.
Hata kama serikali fulani ya Afrika iliharibu uchumi na kuvunja haki za binadamu iliweza kutegemea usaidizi kutoka kwa upande mmoja wa vita baridi ikijitangaza iko upande wake. Siad Barre alikuwa na mapatano na Umoja wa Kisovyeti hivyo Somalia ilihesabiwa kati ya nchi za upande wa Kikomunisti. Baada ya Ethiopia kupatana na Wasovyeti pia tangu mwaka 1974, Somalia iliyokuwa na fitina na jirani yake kuhusu eneo la Ogaden ilihamia upande wa Marekani ikasaidiwa nayo.
Viongozi mbalimbali waliopigania uhuru walipata kimbilio katika nchi za mashariki wakapata nafasi ya kusoma na kujifunza matumizi ya silaha. Hii ilikuwa sababu moja kwa nini wengi walielekea itikadi ya Usoshalisti na kujaribu mbinu za kisiasa na kiuchumi kufuatana na mfano wa Wakomunisti wa Ulaya hata kama siasa yao haikuwa na matokeo mazuri kwao nyumbani.
MWISHO
Mashindano ya kuongeza silaha mpya yalishinda uwezo wa uchumi wa nchi za kikomunisti. Katika miaka ya 1970 ilionekana ya kwamba uchumi wao ulibaki nyuma. Teknolojia mpya hazikuenea kwa sababu utawala wa kidikteta ulijaribu kusimamia mawasiliano yote kwa njia ya polisi na maendeleo yalikwama. Uchumi ulioongozwa na serikali haukuweza kushindana na nguvu ya ubepari.
Umoja wa Kisovyeti ulitia nguvu jeshi na maendeleo ya silaha lakini uwezo wa kiuchumi haukutosha.
Katika miaka ya 1980 ilionekana ya kwamba nchi za mashariki zilibaki nyuma sana. Katika nchi kadhaa wananchi walidai haki za binadamu. Poland iliona harakati ya wafanyakazi waliokataa uongozi wa Wakomunisti wakaanzisha chama cha Solidarnocz na kusababisha utawala wa kijeshi badala ya chama.
Kiongozi mpya wa Umoja wa Kisovyeti Mikhail Gorbachov alielewa hatari ya kuporomoka kwa uchumi wake akatafuta uelewano na Marekani ili kupunguza gharama za jeshi. Siasa mpya ya glasnost iliruhusu kutoa maoni mbalimbali ikaruhusu pia kiwango fulani cha upinzani dhidi ya viongozi. Gorbachov aliamua kutotisha tena nchi zilizoshikamana na Umoja wa Kisovyeti kwa mashambulio ya kijeshi jinsi ilivyokuwa awali.
Hapo nguvu za upinzani zilipata kipaumbele katika nchi kama Hungaria na Poland na viongozi wapya walielekea kuongeza haki za kidemokrasia wakakubali vyama vipya na magazeti huru. Mwaka 1989 wananchi wa Ujerumani ya Mashariki walianza kuandamana wakalazimisha uongozi wa chama cha Kikomunisti kujiuzulu na viongozi wapya walifungua ukuta wa Berlin uliowahi kutenganisha pande mbili za mji huu kwa miaka 38.
Anguko la ukuta wa Berlin lilikuwa dalili ya mwisho wa vita baridi na pia utawala wa Kikomunisti katika nchi za Ulaya. Kote katika nchi za Kikomunistis serikali ilianguka na viongozi wapya walichaguiwa na wananachi. Kufikia mwaka 1991, Wasovieti walichoka kabisa kiuchumi, na vita baridi ikawa imeishia hapo.
Je, Vita Baridi bado inaendelea?
Vita baridi bado inaendelea mpaka leo, hebu tazama Marekani na Korea Kaskazini wanavyotishiana katika umilikii wa silaha nzito nzito, na kurushiana vijembe vya hapa na pale. Watazame tena Marekani na Iran. Aina hii ya vita ipo kabisa, japokuwa upande wa Marekani una unguvu zaidi ikilinganishwa na nchi zilizokuwa za Kisovyeti.

Comments

Popular posts from this blog

KOZI YA KOMPYUTA KWA KISWAHILI

Lies the poor parent tell children